NGARA: Na Shaaban Ndyamukama, DATE.:April 4, 2014
SERIKALI wilayani Ngara mkoani Kagera imewataka wakuu wa shule za sekondari wilayani humo kupeleka majina ya wanafunzi ambao hawajaripoti kuanza kidato cha kwanza kwa maafisa watendaji wa kata ili hatua zichukuliwe kwa wazazi wa wanafunzi hao
Mkuu wa wilaya ya Ngara Costantine Kanyasu amesema hayo leo wakati akiongea na maafisa watendaji wa tarafa na kata kwenye ofisi yake na kudai kuwa muda wa kupeleka watoto shule kwa hiari umeisha tangu machi 31 mwaka huu
Kanyasu amesema kuwa wazazi pia wanatakiwa kuwapeleka shuleni wanafunzi hao kwa kukamilisha ada ya shule vinginevyo katika kuondoa usumbufu wazazi watataifishwa mali zao ili wanafunzi wapate haki ya elimu
“Tumetoa nafasi ya wazazi kupeleka watoto wao shuleni kwa hiari kulingana na baadhi yao kutegemea kuvuna mazao na sasa wanauza badala ya kuwekeza kielimu wanatumia fedha kwenye ulevi sasa hivi ni msako” Alisema Kanyasu
Amesema kuwa katika wanafunzi 2, 770 waliofaulu katika shule 119 za serikali na binafsi wilayani humo kufikia Machi 31mwaka huu ni 70% ya wanafunzi hao ndio wamewasili kwenye shule walizopangiwa na kuanza masomo yao.
Aidha amesema viongozi watakaoshindwa kutumia madaraka waliyopewa kutekeleza maagizo ya serikali basi wajiandae kupoteza nafasi zao kwa kuvuliwa nyadhifa zao kwani serikali imechoka kubembeleza katika utendaji wa umma.